Showing posts with label afya. Show all posts
Showing posts with label afya. Show all posts

Monday, July 15, 2013

ZIFAHAMU NJIA 7 ZA KUPAMBANA NA KIHARUSI (stroke)

KIHARUSI NI NINI?
Ni hitilafu inayotokea kwenye ubongo kutokana na mzunguko wa damu kwenye ubongo kusimama kutokana na kuziba (thrombosis/embolism) au kupasuka(hemorrhage) kwa mishipa inayopeleka damu kwenye ubongo.

Kwa kuwa sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo ubongo zinahitaji uwepo wa damu ili ziweze kufanya kazi, kwa kuwa damu ndiyo inayobeba hewa pamoja na virutubisho, sehemu husika zinazokosa damu zinashindwa kufanya kazi.
Mfano: Ubongo una sehemu maalum ambazo zinahusika na kumwezesha mtu kuongea (speech centers) sehemu hizi zinapokosa damu ya kutosha mtu anashindwa kuongea

AINA ZA KIHARUSI
Kuna aina mbili za kiharusi ambazo ni:
  1. ISCHEMIC STROKE
ni aina ya kiharusi inayosababishwa na kuziba kwa mishipa ya damu iliyoko kwenye ubongo.
Sababu zinazoweza kusababisha mishipa ya damu kwenye ubongo izibe ni pamoja na:
  • Damu kuganda kwenye mishipa ya damu iliyoko kwenye ubongo (thrombosis)
  • Damu kuganda kwenye mishipa ya damu kwenye sehemu nyingine za mwili na kisha damu hiyo kusafirishwa hadi kwenye ubongo (embolism)
  • Kupungua kwa mzunguko wa damu kwenye ubongo
  • Asilimia 30-40% ya  Sababu zinazosababisha aina hii ya kiharusi bado hazijagundulika
    2.  HEMORRHAGIC STROKE

Ni aina ya kiharusi inayosababishwa na kupasuka kwa mishipa ya damu iliyoko kwenye ubongo, kunakosababisha damu kuvuja kwenye ubongo.
Damu inayovujia kwenye ubongo husababisha mgandamizo (compression) ambao unaweza ukasababisha damu isiweze kupita vizuri kwenye ubongo na hivyo kufanya sehemu za ubongo kutokupata hewa na virutubisho

DALILI ZA KIHARUSI

Dalili za kiharusi huwa zinaanza muda mfupi sana (dakika au sekunde chache) kabla ya mtu kupata madhara, Dalili hizo hutegemea na sehemu ya ubongo ambayo imeathirika.
  • Kukosa nguvu kwa misuli ya uso
  • Kushindwa kuongea na kusikiliza maongezi kwa ufasaha
  • Kuyumba wakati wa kutembea (balance problems)
  • Kuongezeka kwa mapigo ya moyo
  • Kupoteza kumbukumbu mara kwa mara
  • Kushindwa kuona vizuri
  •  Maumivu ya kichwa( kwa wenye hemorrhagic stroke

NJIA ZA KUGUNDUA UWEPO WA KIHARUSI

Kiharusi hupimwa kwa kutumia CT-scan, MRI-scan pamoja na njia nyingine kulingana na maelekezo yatakayotolewa na daktari

VISABABISHI VYA KIHARUSI (risk factors)

Sababu zifuatazo zinaweza kusababisha kiharusi:
  • Kisukari
  • Ukosefu wa mazoezi
  • Matumizi ya nyama nyekundu za kwenye makopo kwa muda mrefu
  • Matumizi ya madawa ya kulevya (cocaine na amphetamines)
  • Uvutaji wa sigara
  • Ulevi wa kupindukia
  • Matumizi ya muda mrefu wa baadhi ya madawa ya kikohozi yenye kemikali ziitwazo symphathomimetics
  • Vyakula vyenye mafuta mengi husababisha ugandaji wa mafuta kwenye mishipa (cholesterol) na hivyo kufanya mishipa ya damu kuwa myembamba (atherosclerosis) 
  • Uzee
NJIA ZA KUPAMBANA NA KIHARUSI
Chakula bora ni njia rahisi zaidi na salama ya kujikinga na kiharusi. Baadhi ya njia za kupambana na kiharusi ni hizi zifuatazo: 
  • Tumia mafuta ya kupikia yatokanayo na vitu asilia kama vile mafuta ya karanga, mafuta ya ubuyu, mafuta ya alizeti, mafuta ya mizeituni (olive oil)
  • Kula matunda na mbogamboga kwa wingi
  • Tumia nafaka zisizokobolewa (unpolished cereals)
  • Tumia nyama nyeupe (samaki,dagaa,kuku) kwa wingi
  • Punguza matumizi ya nyama nyekundu (ng'ombe, kondoo nk) 
  • ASPRIN huwa inapunguza uwezekano wa kupata kiharusi
  • Tumia mafuta yasiyo na lehemu (cholesterol)
Kutokana na ukweli kwamba mara nyingi kiharusi hakina dalili mpaka kianze kuleta madhara makubwa, ni vizuri kwenda kuwaona wataalamu wa afya  kwa uchunguzi pamoja na ushauri zaidi.

Watu waliogundulika kua na kiharusi wanapaswa kumwona daktari haraka kwa matibabu pamoja na ushauri zaidi

vyanzo:
Center for Disease Control (CDC)
bbc/health
stanford.edu