Sunday, July 7, 2013

MADHARA YA KISUKARI

KISUKARI

KISUKARI NI NINI?


Kisukari ni ugonjwa unaosababisha kupanda kwa kiasi cha sukari kwenye damu. Chakula tunachokula huwa kinabadilishwa kuwa sukari ili tupate nguvu. Pamoja na umuhimu huo wa sukari katika miili yetu, kiasi cha sukari kinatakiwa kidhibitiwe ili kisizidi kiasi ambacho kinaweza kuleta madhara mwilini. Kongosho, linalopatikana karibu na tumbo ndilo linalohusika katika kudhibiti kiasi cha sukari mwilini kwa kutoa homoni inayoitwa insulin. Kongosho linaposhindwa kufanya kazi kiasi kikubwa cha sukari kinabaki kwenye damu na kinaweza kikaonekana kwenye mkojo pia.
Sukari inapozidi kwenye damu, mtu anaweza kupata madhara mengi kama vile matatizo ya moyo, matatizo ya figo, kutokwa na damu isiyokatika na hata upofu.
Ugonjwa wa kisukari haukua umeenea sana miaka iliyopita ila kwa sasa umeongezeka kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha.

DALILI ZA KISUKARI

Mtu mwenye kisukari anaweza akawa na dalili zifuatazo:
  • Kukojoa mara kwa mara
  • Kusikia kiu kali mara kwa mara
  • Kupungua uzito
  • Njaa mara kwa mara
  • Matatizo ya kuona
  • Miguu na vidole kufa ganzi
  • Uchovu wa mwili
  • Kukauka kwa ngozi
  • Vidonda kuchelewa kupona
  • Kushambuliwa na magonjwa mara kwa mara

Kwa watu walioshambuliwa na kisukari kwa muda mrefu kutapika na  kichefuchefu vinaweza vikawashambulia pia

AINA ZA KISUKARI

Type 1 diabetes:
Ni aina ya kisukari ambayo kongosho linakua linashindwa kutengeneza homoni ya insulin. Ni aina ya kisukari ambacho kinawapata watu wachache kuliko aina nyingine ya kisukari. Ni asilimia tano 5% tu ya watu wote wenye kisukari wana aina hii ya kisukari.

Type 2 diabetes
 ni aina ya kisukari ambacho kinatokana na mwili kushindwa kutumia homoni ya insulini, watu wenye aina hii ya kisukari mara nyingi hawana matatizo yoyote kwenye kongosho, ila ni miili yao tu inashindwa kutumia homoni ya insulin
Kisukari cha uzazi(Gestational diabetes)
Ni aina ya kisukari kinachowapata akina mama wajawazito pekee. Endapo aina hii ya kisukari itachelewa kutibiwa inaweza kusababisha matatizo kwa mama pamoja na mtoto aliyeko tumboni, hivyo ni muhimu kwa akina mama kuhudhuria clinic kipindi cha ujauzito
Aina hii ya kisukari huwa kinawapata asilimia mbili (2%) ya akina mama wajawazito na huwa kinatoweka baada ya kujifungua.

VISABABISHI VYA KISUKARI
  • Kisukari kinaweza kupatikana kwa kurithi.
  • Unene uliopitiliza (kuongezeka uzito)
  • Kutokufanya mazoezi
  • Wanawake waliowahi kupata kisukari wakatiwa ujauzito wao wana hatari kwa 60% kupata type I au type II diabetes kwenye maisha yao.
  • Watu wenye umri zaidi ya miaka 40 wana hatari zaidi ya kupata ugonjwa wa kisukari
  • Watu ambao familia zao zina historia ya kupata kisukari pia wana uwezekano mkubwa wa kupata kisukari
 Sababu nyingine za kisukari bado hazitambuliki kwa sasa, ila zinafanyiwa utafiti
NJIA ZA KUZUIA KISUKARI
Njia nyingi zinazoweza kusaidia kupunguza hatari ya kupata kisukari zinahusisha kubadilisha mfumo wa maisha. Njia hizo ni pamoja na:

  • Fanya mazoezi mara kwa mara
  • Punguza matumizi ya sukari
  • Punguza matumizi ya mafuta mengi na chumvi kwenye chakula 
  • Kula matunda na mboga mboga kwa wingi
  • Epuka kutumia vyakula na vinywaji vyenye sukari nyingi kama soda, biskuti na pipi mara kwa mara
  • Punguza matumizi ya pombe
  • mwone daktari mapema pindi unapohisi una dalili za kisukari. Hii itasaidia kupunguza hatari ya kupata matatizo mengine yanayo ambatana na kisukari
MATIBABU YA KISUKARI
  • KWA WENYE TYPE I DIABETES:
 Huwa wanachomwa sindano ambazo zina homoni ya insulini ambayo inatengenezwa kiwandani (synthetic insulin)
  • WENYE TYPE II DIABETES
 Hutumia dawa iitwayo metformin

TAHADHARI: Dawa hizi zote zinatumika kulingana na maelezo ya daktari, muone daktari kabla ya kuamua kutumia dawa za kisukari kwani matumizi mabaya ya dawa huwa yanasababisha madhara mwilini

KISUKARI KINAWEZA KUWAPATA WATOTO?
Ilikuwa ikiaminika kuwa watoto huwa hawana hatari ya kupata kisukari, ila na watoto nao wanaweza kupata kisukari na hivyo basi ni muhimu kwa watoto nao kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu endapo itapatikana kuwa wana kisukari.

Vyanzo:
Center for Disease Control (CDC)
http://www.mayoclinic.com
http://www.bbc.co.uk/news/health

No comments:

Post a Comment