Sunday, January 19, 2014

MATUMIZI SALAMA YA ASPIRIN

Aspirin ni dawa inayotumika kutuliza maumivu na uvimbe(inflammation)  katika mwili. Dawa hii pia hutumika kutuliza homa pamoja na  kuzuia matatizo ya moyo(atherosclerotic plaque), saratani ya utumbo mpanana(colorectal cancer),  kiharusi endapo daktari ataona ni vema. Aspirin hutumika kutuliza maumivu ya kichwa, mgongo,meno, misuli na mengine yanayofanana na hayo. madhara(side effects) za aspirin zinatofautiana kulingana na umri, hali ya kiafya pamoja na kiasi cha dawa kilichotumika.
1. WATOTO
Aspirini haishauriwi kutumika na watoto wadogo kwani zinaweza kusababisha ugonjwa uitwao Reye's syndrome. Ugojwa huu mara nyingi huwapata watoto wenye umri chini ya miaka 12 ambao wanatumia aspirin mara kwa mara. Imegundulika kwamba watoto wenye magonjwa kama tetekuwanga wana hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa huu baada ya kutumia aspirin. Ugonjwa huu hushambulia ini na ubongo na unaweza kusababisha kifo kama mtoto hatapata matibabu haraka.

Dalili za Reye's syndrome ni pamoja na:
  • Kutapika mara kwa mara
  • Mabadiliko ya tabia
  • Kuzubaa
  • Kupumua haraka haraka(hyperventilation)
Dalili hizi hutokea baada  tu ya kupona ugonjwa wa mafua au tetekuwanga.
Uwepo wa ugonjwa huu unaweza kugundulika kwa kupimwa damu au mkojo na matibabu ya haraka yanahitajika ili kuzuia madhara makubwa zaidi kwenye ubongo pamoja na ini ambayo yanaweza kusababisha kifo. 

2. VIDONDA VYA TUMBO(ulcers)
Inashauriwa watu wenye vidonda vya tumbo wasitumie Aspirin kwani inaweza kuongeza tatizo hilo na hata kusababisha uvujaji wa damu tumboni. Dawa mbadala kama vile paracetamol inaweza ikatumika kutuliza maumivu badala ya aspirin kwa mtu mwenye vidonda vya tumbo kwa kuwa aspirin ina asili ya tindikali(acidic). 

3. KIUNGULIA(heart burn)
Kwa kuwa aspirin huongeza kiasi cha tindikali tumboni, kiasi kidogo cha tindikali hiyo hurudi kwenye koo la chakula na kusababisha mtu apate kiungulia.

4. KUVUJA DAMU KWENYE UBONGO(Cerebral hemorrhage)
 Moja wapo kati ya kazi za aspirin ni kuzuia damu kuganda(anti-clotting) na hivyo huweza kusababisha kuvuja kwa damu kwenye ubongo.
  • Watu wanaotarajia kufanyiwa upasuaji wanashauriwa wasitumie aspirin kwa kuwa inaweza ikasababisha wavuje damu nyingi wakati wa upasuaji.
5. ALEJI (allergy)
Baadhi ya watu hupata madhara baada ya kutumia aspirin. Baadhi ya dalili za kuwa na aleji ya aspirin hutokea lisaa limoja baada ya kumeza kidonge cha aspirin nazo ni ni pamoja na:
  • Kuwashwa kwa ngozi pamoja na kutokwa na vipele(skin rashes)
  • Kushindwa kupumua vizuri(pumu/asthma)  
 6. KUTUMIA KIASI KIKUBWA CHA ASPIRIN (aspirin poisoning/salycilism)
 Kama zilivyo dawa zingine, matumizi makubwa ya dawa hii huifanya iwe sumu mwilini(intoxication). Sumu zilizoko mwilini huchujwa kwenye ini ila, ini huzidiwa kama kiasi cha sumu kikizidi. Matumizi ya aspirin kwa muda mrefu pia huweza kusababisha magonjwa ya ini pamoja na figo. Dalili zake hutegemea na kiasi pamoja na muda wa matumizi, 
Madhara yatokanayo na matumizi ya kiasi kikubwa cha aspirin kwa muda mfupi(Acute aspirin poisoning )
  • Maumivu makali ya tumbo
  • Kichefuchefu na kutapika
Madhara yatokanayo na matumizi ya kiasi  kidogo cha aspirin kwa muda mrefu(Chronic aspirin poisoning )
  • Uchovu
  • Kutetemeka(seisures)
  • Moyo kwenda mbio
  • Kupumua kwa kasi(hyperventilation)
MUINGILIANO NA DAWA NYINGINE
  • Kwa wanaotumia dawa za kisukari, aspirin inaweza ikasababisha sukari kushuka kupita kiasi (hypoglycemia) 
  • Kwa wanaotumia aspirin ili kuzuia matatizo ya moyo au kiharusi, hawatakiwi wachanganye pamoja na dawa zingine za maumivu kama ibuprofen
  • Madhara ya aspirin huongezeka pale inaponywewa pamoja na pombe, kwani husababisha damu kuvuja kwa wingi tumboni kwa watu wenye vidonda vya tumbo
MATUMIZI SALAMA YA ASPIRIN
  • Ili kupunguza hatari ya kupata vidonda vya tumbo, usitafune aspirin, meza kama ilivyo.
  • Meza aspirin kwa angalau glass moja ya maji
  • Usivunje wala kusaga kidonge cha aspirin kabla ya kumeza
  • Hakikisha unamtaarifu daktari wako kama unatumia aspirin kabla ya upasuaji/operesheni(surgery)
  • Watoto wa chini ya miaka 12 wasitumia aspirin pasipo ushauri wa daktari
  • Usitumie vidonge vya aspirin vyenye harufu ya siki(vinegar) kwani vinaashiria kuwa vimeisha muda wake
SOURCES

No comments:

Post a Comment